Friday, October 21, 2016

JOHANNESBURG YAFANA AFRIKA NZIMA YAHAMIA PALE KUSHUHUDIA TUZO ZA MTV (MTV AFRICA MUSIC AWARDS).

14564865_350361321967099_6036778535429865472_n
Ni tuzo kubwa na zinazosherehekewa zaidi kuliko zote barani Afrika. Ni tuzo zenye heshima zaidi na maandalizi yake hujumuisha mbwembwe za kila aina.
MTV MAMA 2016, kwa mara nyingine tena inawakutanisha wababe wote wa muziki barani Afrika kwenye jukwaa moja. Mwenyeji mwaka huu, ni jiji la Johannesburg, jijini Afrika Kusini, likipokea kijiti kutoka kwa mji wa Durban uliopata bahati ya kuziandaa kwa miaka miwili mfululizo,
Macho na masikio ya Waafrika wengi sasa yanaelekezwa huko na kila nchi yenye wawakilishi ikiomba warudi na tuzo nyumbani – waipe heshima nchi yao.
Ukitoa Afrika Kusini na Nigeria zenye wasanii wengi zaidi waliotajwa kuwania, Tanzania nayo inashikilia nafasi ya juu kwa uwakilishi. Diamond, Alikiba, Vanessa Mdee, Yamoto Band, Navy Kenzo na Raymond, wameifanya Tanzania iwe na wawakilishi 6 mwaka huu – si haba na ni ishara kubwa kuwa muziki wetu unazidi kuwa na nguvu.
Kama hiyo haitoshi, jukwaa la MAMAs litapandwa na wasanii wawili wa Bongo Flava, Diamond na Alikiba, mahasimu wanaotengeneza pande mbili za mashabiki wanaosigana kila leo. Uwepo wa wawili hao kwenye tuzo hizo mwaka huu tena wakishare jukwaa moja, kunazifanya tuzo hizo mwaka huu ziwe za aina yake.
Kuna muitikio mkubwa pia wa wasanii wengine wa Tanzania katika kuwaunga mkono wasanii wote waliotajwa mwaka huu. Yapo matarajio makubwa kuwa huenda nusu ya wasanii hao waliotajwa mwaka huu, wanaweza kuja na ushindi nyumbani. Kila lakheri kwa wote.

No comments:

Post a Comment