Manchester United hawana Vidal,Marchisio wala Pirlo katika kikosi chao lakini kimebarikiwa kuwa na utajiri wa watu tofauti tofauti katika eneo la kiungo. Wana Herrera,Schneiderlin,Fellaini na Carrick huku nguvu ikiongezwa na usajili ghali zaidi duniani wa Paul Pogba.
Pogba ameingia moja kwa moja kwenye kikosi cha United lakini ni nani anaweza kumfanya Pogba akae sawa katika kikosi hiko!? Mourinho anaumia kichwa kuliko hata tunavyomuona akitabasamu kuhusu kikosi chake kilivyo.
Kwa muda mfupi tu Pogba amecheza na Fellaini,Schneiderlin na Herrera lakini hakuna ambaye anarandana naye pale katikati. Fellaini ni mmoja wa waliocheza na Pogba mechi nyingi lakini hampi kile kilicho bora sababu Fellaini si mzuri katika kuchezesha wengine vivyo hivyo kwa Schneiderlin.
United wamekosa ubunifu eneo la katikati hamna mtu ambaye anafanya kazi ya kuiunganisha timu. Mbinu kubwa ya timu hiyo ni kutumia mbio za Valencia na Shaw katika kutengeneza nafasi za magoli kwa hali hiyo huwezi kuona ubora wa Pogba ambaye muda mwingi anakuwa yupo katikati kusubiri mipira ambayo inakimbizwa pembeni.
Scholes amefunguka na anaamini back up nzuri ya Pogba ni Carrick. Kwa asilimia 90 natembea pamoja na Scholes sababu Carrick ni mtu tofauti kabisa ukimuweka kundi la Fellaini na Schneiderlin. Licha ya umri kuwa mkubwa United bado wanamuhitaji katika kuifanya timu hiyo iwe na uwiano katika eneo la kiungo.
Ufanisi wa kupiga pasi ndefu,fupi na zile za kupenyeza kwa mshambuliaji ndio ubora wa Carrick ulipo. Miguu yake ina macho kuliko Schneiderlin na Fellaini hata Herrera ambaye muda mwingi anapiga pasi za pembeni. Kombinesheni ya Carrick na Pogba inaweza kuwa bora kwa United kuzinduka upya.
Mourinho inabidi ampe Carrick nafasi sasa sababu ana mbinu mbadala za kumkabili mpinzani kwa uwezo wake wa kuusoma mchezo na kuwachezesha wenzake. Muda mwingi Pogba amekuwa anarudi sana nyuma kufuata mipira, sasa uwepo wa Carrick utamfanya Pogba awe na ziara chache za kurudi nyuma hapo ndipo ubora wake unaweza kuonekana.
Mourinho mfungulie Carrick ili uondoe aibu ya Pogba. Carrick ndiye mwenye ufunguo halisi wa kumfungulia dunia Pogba na kuwa anachokitaka japo Mourinho anamuondoa taratibu Carrick kwenye kikosi.
No comments:
Post a Comment